”THE PRESIDENTIAL TOUR” YA RAIS SAMIA YAVUTIA WANAWAKE ZAIDI YA 400 HIFADHI YA TAIFA ARUSHA"
Na. Edmund Salaho/ Arusha
Zaidi ya wanawake 400 washerehekea siku ya wanawake duniani katika Hifadhi ya Taifa Arusha. Leo tarehe 09, Machi Jeshi hilo la wanawake limetua katika Hifadhi ya Taifa Arusha kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuitangaza nchi yetu.
Mhe.Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi, Rais wa Zanzibar, wameshiriki kuitangaza Tanzania mahsusi kwa soko la China walipomkaribisha nchini staa wa filamu za Kichina, Bw. Jin Dong na kurekodi filamu hiyo ambayo itatoka mapema mwaka huu
Akizungumza wakati wa kuwakaribisha wanawake hao katika Hifadhi ya Taifa Arusha, Mkuu wa Hifadhi ya Arusha, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Yustina Kiwango aliwapongeza wanawake kwa moyo na jitihada za kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Napenda kuwakaribisha katika hifadhi ya Taifa Arusha wanawake ni jeshi kubwa leo mmedhihirisha hilo kwani wanawake hatuna jambo dogo leo mmekanyaga mahali alipokanyaga jemedari namba moja Rais Samia alichokiona na kukitangaza leo tutakiona ujio wenu kama Jeshi la wanawake ni matokeo makubwa ya “Royal Tour” na The “Presidential Tour” alisema Kamishna Kiwango
Itakumbukwa Agosti 20, 2023 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan alifanya filamu maarufu kama “The Presidential Tour” wengi hupendelea kuiita Royal tour ya pili ambayo imekuwa ikivutia idadi kubwa ya watalii katika Hifadhi za Taifa nchini hususani Hifadhi ya Taifa Arusha.
Katika ziara hiyo ya kutembelea Hifadhi ya Arusha wanawake walipata fursa ya kutalii na kujionea vivutio mbalimbali katika hifadhi hiyo ikiwa ni pamoja na kufahamu fursa za uwekezaji zinazopatikana katika Hifadhi ya Taifa Arusha.
Comments