TANAPA YAPOKEA MITAMBO NA MALORI YENYE THAMANI YA SHILINGI BILIONI 6.4 KUBORESHA MIUNDOMBINU HIFADHI ZA TAIFA SERENGETI NA NYERERE

 Na Philipo Hassan/ Dar es salaam

Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) amewakabidhi TANAPA Malori matano na mitambo mitano yenye thamani ya Dola milioni 2.4 sawa na shilingi Bilioni 6.4 za Kitanzania, tukio hilo limefanyika leo Disemba 2, 2024 katika Ukumbi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (Mpingo House) jijini Dar es salaam.


Vifaa hivyo viliyonunuliwa kupitia mradi wa Dharura kwa Uhifadhi na Utalii Tanzania (Emergency Recovery Support for Biodiversity in Tanzania) kupitia benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW).


Akizungumza katika makabidhiano haya Balozi Dkt. Chana alieleza kuwa vifaa hivyo vitaboresha shughuli za Uhifadhi pamoja na miundombinu katika Hifadhi za Taifa Serengeti na Nyerere kwa malengo ya kupunguza athari zilizosababishwa na janga la UVIKO-19 kwenye Utalii na Uhifadhi.

Dkt. Chana alisema “Nawaagiza Bodi na Wakuu wa Mashirika ya TANAPA na TAWA kuhakikisha kuwa vitendea kazi hivi vinatumika kufanya kazi zilizokusudiwa za Uhifadhi wa Maliasili na Utalii na vinatunzwa ipasavyo kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na taratibu za matumizi ya vifaa vya Serikali.”


Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhanini TANAPA Jenerali mstaafu George Waitara alishukuru Serikali ya Ujerumani kwa kuendelea kusaidia uhifadhi nchini Tanzania hasa katika miradi ya dharura. 


“Msaada huu wa dharura umetuwezesha kuvuka kipindi cha dharura ya uviko 19 katika Uhifadhi na kuendelea kuimarisha miundombinu yetu bila kuyumba. Kwa kufanya hivyo, mifumo ya Ikolojia iliendelea kushamiri ndani ya Hifadhi za Taifa nchini.


Mkurugenzi Mkazi wa Frankfurt Zoological Society (FZS) Tanzania, Dkt. Ezekiel Dembe alieleza mafanikio ya miradi mbalimbali inayotekelezwa Tanzania kwa kusema “Frankfurt Zoological Society  imekuwa Tanzania kwa zaidi ya miaka 65 kwamba tunajivunia kufanya kazi na Wizara ya Maliasili na Utalii, TANAPA, TAWA na wadau wengine wote tunaofanya nao kazi kwa sababu wamekuwa wakitekeleza makubaliano ya mikataba  ipasavyo”.


Mradi wa Usaidizi wa dharura kwa Uhifadhi na Utalii nchini Tanzania umesaidia juhudi za kutoa msaada wa haraka na mipango ya muda mrefu ya kurejesha na kulinda mifumo ikolojia mbalimbali ya Tanzania, hasa pale ambapo vitisho vikubwa kama mabadiliko ya tabianchi, ujangili, au majanga ya asili yanayosababisha uharibifu kwa wanyamapori na makazi yao, juhudi za mradi zinahusisha ushirikiano kati ya serikali ya Tanzania na Ujerumani, Shirika la Frunkfurt Zoological Society pamoja na jamii za wenyeji ili kudhibiti na kuimarisha ustahimilivu wa bioanuwai nchini.











Comments

Popular posts from this blog

KUNDI LINGINE LA WANANCHI 541 LAHAMA NGORONGORO

𝐔𝐉𝐄𝐍𝐙𝐈 𝐖𝐀 “𝐒𝐄𝐑𝐄𝐍𝐆𝐄𝐓𝐈 𝐍𝐀𝐓𝐈𝐎𝐍𝐀𝐋 𝐏𝐀𝐑𝐊 𝐆𝐎𝐋𝐅 𝐂𝐎𝐔𝐑𝐒𝐄” 𝐖𝐀𝐅𝐈𝐊𝐈𝐀 𝐀𝐒𝐈𝐋𝐈𝐌𝐈𝐀 𝟒𝟐

UTALII WA MALIKALE WASHIKA KASI NCHINI, WAFARANSA WAFURIKA KILWA KISIWANI