SIX RIVER AFRICA NA ECO WASHIRIKIANA NA TANAPA KUBORESHA HUDUMA ZA MATIBABU YA WANYAMAPORI


Na. Happiness Sam- Same


Shirika la Six Rivers Africa pamoja na Elephant Conservation Organisation (ECO) yameungana na TANAPA ili kuimarisha huduma za matibabu ya wanyamapori katika hifadhi za kanda ya kaskazini kwa kuongeza vitendea kazi ikiwemo gari, vifaa tiba pamoja na dawa za kutibu wanyamapori ili kuhakikisha ustawi wa wanyamapori unaimarika katika maeneo hayo.


Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Tiba ya Wanyamapori, jana Februari 18, 2025 katika Hifadhi ya Taifa Mkomazi iliyopo Wilaya ya Same, Mkoani Kilimanjaro, Mkuu wa wilaya ya Same Kasilda Mgeni alieleza umuhimu wa uhifadhi kwa maendeleo ya taifa kwani unasaidia katika kutunza urithi wetu wa asili ikiwemo wanyamapori kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vizazi vijavyo.



DC Mgeni alisema  “Mradi wa Tiba ya Wanyamapori (Veterinary Support Project) ulianzishwa mwaka 2013 katika Hifadhi yetu ya Taifa ya Mkomazi kwa lengo la kuchukua hatua muhimu katika kuhakikisha mafanikio endelevu ya juhudi zetu za uhifadhi, mradi huu utaimarisha huduma za wanyamapori katika hifadhi yetu hii pamoja na hifadhi nyingine za kanda ya kaskazini.”


Aidha, DC Mgeni alitoa shukrani kwa shirika la Six Rivers Africa, Elephant Conservation Organisation(ECO) pamoja na TANAPA kwa jitihada zao za kuimarisha ustawi na mafanikio ya hifadhi , uongozi wao katika kutekeleza miradi pamoja na juhudi zao za kuimarisha afya ya wanyamapori hivyo kuchochea mafanikio makubwa katika uhifadhi wa wanyamapori nchini.


Akimwakilisha Kamishna wa Uhifadhi Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania TANAPA,Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Sonia Lyimo, alisema kuwa mradi huo utaongeza uwezo wa kulinda na kutunza afya za wanyamapori katika hifadhi zetu ili wanyama wetu waweze kuishi maisha bora pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zinazoweza kuhatarisha afya ya wanyamapori.




Kamishna Lyimo aliongeza kuwa “ Mradi huu utaleta mabadiliko makubwa sio tu kushughulikia changamoto katika huduma za tiba ya wanyamapori na urejeshaji wa wanyamapori bali pia kusaidia kuendeleza maisha ya jamii zinazozunguka hifadhi za kanda ya kaskazini”.


Kwa upande wake, Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Six River Africa Brandon Kemp, alisema wametoa msaada huo ili kuunga mkono juhudi za serikali ya Tanzania katika kuhakikisha Hifadhi za Taifa zinalindwa pamoja na kusaidia shughuli nyingine za kiuhifadhi.




Shirika la Six River Afrika kwa kushirikiana na Elephant Conservation Organisation (ECO) wametoa gari aina ya “Toyota Land Cruiser” maalumu kwa shughuli za mradi huo, sambamba na vifaa vilivyogharimu shillingi millioni 140 ikijumuisha seti ya zana zkutolea huduma ya tiba pamoja na matibabu  ili kulinda na kutunza afya za wanyamapori katika Hifadhi ya Taifa Mkomazi, Arusha, Kilimanjaro, Tarangire na Manyara.








Comments

Popular posts from this blog

KUNDI LINGINE LA WANANCHI 541 LAHAMA NGORONGORO

𝐔𝐉𝐄𝐍𝐙𝐈 𝐖𝐀 “𝐒𝐄𝐑𝐄𝐍𝐆𝐄𝐓𝐈 𝐍𝐀𝐓𝐈𝐎𝐍𝐀𝐋 𝐏𝐀𝐑𝐊 𝐆𝐎𝐋𝐅 𝐂𝐎𝐔𝐑𝐒𝐄” 𝐖𝐀𝐅𝐈𝐊𝐈𝐀 𝐀𝐒𝐈𝐋𝐈𝐌𝐈𝐀 𝟒𝟐

UTALII WA MALIKALE WASHIKA KASI NCHINI, WAFARANSA WAFURIKA KILWA KISIWANI